2014 KCSE Kiswahili Past Paper-Free KCSE Past Papers with Answers.

2014 KCSE Kiswahili Past Paper

KISWAHILI

Karatasi ya 1

INSHA

1 Lazima

Andika hotuba utakayowatolea wazazi, walimu na wanafunzi kuhusu umuhimu wa ushauri/nasha katika shule za sekondari.

2 Andika insha kuhusu jinsi raia wanavyoendeleza matumizi mabaya ya ardhi nchini.

3 Andika kisa kitakachodhihirisha maana ya methali: Achanikaye kwenye mpini hafi njaa.

4 Tunga kisa kinachoanza kwa maneno yafuatayo

Mara tu nilipokivuka kizingiti cha lango la nyumba yangu, nilijua kwamba maisha yangu yalikuwa yanachukua mkondo mpya

KISWAHILI

Karatasi ya 2

LUGHA

UFAHAMU: (Alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Afisa wa ukaguzi wa abiria na mizigo alimrudishia cheti chake cha usafiri na kubofya tarakilishi yake kuashiria kuanza kumhudumia mteja mwingine. Duma alikichukua cheti chake cha usafiri kwa pupa, kana kwamba anamtarajia mtu kuja kukibwakura. Moyo wake ulitweta na kukisukuma kidari chake kikembe nusura kukipasua. Baada ya kukihifadhi cheti hiki ndani ya mfuko Wake mdogo wa kusafiria, alichapuka moja kwa moja hadi chumbani ambamo wasafiri hungojea kuiva kwa safari.

Si kwamba Duma ni mwanagenzi wa safari za Ughaibuni. La! Hasha. Amekia vilele vya anga kwa muda Wa miaka isiyopungua kumi sasa, tangu alipochukuliwa kijijini mwao akiwa na umri wa miaka kumi na miwili; mjomba wake anakuja kumtafutia kazi. Kazi aliyopata ilimtia tumbo joto mwanzoni, akataka kutoroka, atokomee kokote kule. Fikiria wewe, ndio sasa umetoka kwenye mbeleko ya mama yako, ubwabwa Wa shingo ndio unaanza kukutoka, kisha uje kutoswa kwenye kazi ya kuvuna majani kwenye shamba kubwa la Bwana Mali, majani ambayo unapopata fursa ya kuyatafuna yanakufanya kujihisi kama tiara inayoelea angani! Kisha baadaye upagazwe kazi ya kuyauza majani hayo hayo, pamoja na unga unaohifadhiwa katika vifuko vidogo vya kuvutia, kwenye soko la siri na hata shuleni! Hata hivyo walisema wasemao kwamba papo kwa papo kamba hukata jiwe, na kinolewacho hupata.

Duma alipata walimu, akafunzwa jinsi ya kuyatumia majani na aina mbalimbali za unga ili kuituliza nadhari na dhamiri yake ambayo awali ikimsumbua sana. Polepole ule utu na ulimbukeni aliokuwa nao uliyeyuka, akatwaa moyo wa jiwe na kuikumbatia kazi hii kwa dhati ya moyo wake, moyoni akijiambia kuwa hayo ndiyo majaliwa yake. “Ikiwa huu si utashi wa Mungu, kwa nini akalituma gonjwa kuja kuwaua wazazi wangu, mmoja baada ya mwingine? Kwa nini akawaacha akina ami kunipoka kidogo kilichobakizwa na matibabu ya Wazazi Wangu? Kwa nini asimtume mtu kuja kuniokoa nilipoingizwa kwenye biashara hii na mjomba Papa?” Duma alijiuliza maswali haya mfululizo. Hatimaye aliihalalisha kazi yake kwa kusema, “Kazi mbi si mchezo mwema.”

Duma alipopata tajiriba ya kutosha kupambana na walinda usalama wenye macho ya kipanga, mwajiri wake hakusita kumturnia kwenye safari za kusafirisha shehena kwenye masoko ya ng’ambo. Mara nyingi aliponea tundu la sindano kutiwa mbaroni. Wakati mwingine mashine za ukaguzi ziliweza kunusa shehena yake, akalazimika kulainisha viganja vya maafisa wakuu wa forodha. Kila mara alijiambia, “Hii kazi ni hatari, nikipata pesa za kutosha kuufukuza uhawinde nitang’atuka.” Hata hivyo, Duma tayari alikwisha kuwa sikio la kufa. Alikuwa amedidimia katika ulanguzi wa dawa za kulevya, ulanguzi ambao ulikuwa umemwingia kwenye mishipa jinsi dawa zenyewe zilivyokuwa zimegeuka damu inayousukuma moyo wake. Badala ya kuacha, yeye na mwajiri wake walizua mikakati mipya ya kusafirisiha shehena.

Safari ya leo ilipoiva, Duma alifanya kama alivyoagizwa na mwajiri Wake. Asubuhi na mapema alibugia shehena yake, koo ikakubali kuisafirisha hadi tumboni ambapo uchango wake uliombwa kuihifadhi hadi utakapofika Wakati wa kuitapika shehena hiyo Ughaibuni. Fungu lililobaki lilitiwa ndani ya begi la kusafilia, katikati ya nguo. Duma alitarajia kwamba atampata jamaa wake wa kawaida kwenye forodha. Akajiambia kwamba hata asipompata huyo jamaa anaweza kuitoa shehena hiyo hiyo kama kafara kwa maafisa wa usalama. Duma alikuwa na bahati ya mtende kumpata huyo jamaa Wake, pamoja na afisa wa usalama aliyejuana naye kwa vilemba, akafanikiwa kupitisha shehena zake bila kujua kwamba yake ya arubaini imefika

Mara tu Duma alipotua kwenye uwanja wa ndege wa Kainata, Polisi Wa Kimataifa Walimzingira. Mimweko ya kamera za Wanahabari ilitishia kuyapofua macho ya mtumwa huyu ambaye alikuwa sharti auawe kwa kukubali kutumwa. Vikuku viwili vikubwa vilivirembesha viwiko vya mikono yake ambayo aliikabidhi kwa maafisa hawa kama anayekubali kuwajibikia kosa lake. Nchini mwake mwajiri Wake alipiga kidoko alipotazama kadhia hii kwenye runinga. Akasema, “Bloody coward! How could he allow himself to be caught? ”

(a) Huku ukitoa mifano mitano, onyesha jinsi haki za kibinadamu zilivyokiukwa katika kifungu hiki. (alama 5)

(b) Andika vyanzo vinne vya maovu ya kijamii kwa mujibu wa taarifa. (alama 4)

(c) “Yaliyompata Duma ni mwiba wa kujichoma.” Thibitisha kauli hii kwa kutoa mifano minne. (alama 4)

(d) Eleza maana za msamiati ufuatao kulingana na kifungu: (alama 2)

(i) wenye macho ya kipanga

(ii) zimegeuka damu inayousukuma moyo wake

2. UFUPISHO: (Alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Suala la jamii kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula na lishe ni jambo ambalo halina budi kushughulikiwa kwa dhati. Chakula ni mojawapo ya mahitaji ya kimsingi ya binadamu na kila mja ana haki ya kupata chakula, na si chakula tu, bali chakula chenye virutubisho muhimu. Nchi isiyowakimu raia Wake kwa chakula ni sawa na ng’ombe aliyeshindwa kunmyonyesha ndama wake.

Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la ukosefu wa chakula. Msimu wa kiangazi unapobisha hodi, watu wengi, hasa Wale wahitaji, hupukutika kutokana na mng’ato wa njaa. Japo serikali na Wafadhili hutuma vyakula vya msaada kwa jamii zilizoathirika zaidi, chakula hiki huwa kama nguo ya kuazima, na bila shaka ya kuazima haikidhi haja.

Mojawapo ya vyanzo vikuu vya uhaba wa chakula ni kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi wa chakula chenyewe. Zipo sehemu nyingi nchini ambazo ni kame. Sehemu hizi hukabiliwa na ukosefu Wa maji kwani, ama mvua hainyeshi, au inaponyesha haitoshelezi mahitaji ya mimea. Mimea mingi hujikaukia ikiwa michanga na kudhihaki juhudi za wapanzi. Zipo sehemu katika nchi hii ambazo huenda kwa misimu hata zaidi ya mitano bila kupata zao lolote kutoka mashambani. Hali ikiwa hivi makali ya uhitaji huzidi na wakazi wa sehemu hizi hulazimika kuwa wategemezi kwa majirani na serikali. Wengine wanapokosa chakula kabisa huazimia kula visivyoliwa. Wanaamwa la mbwa baada ya kukosa la mama.

Hali kadhalika, japo zipo sehemu nyingine ambazo hazina tatizo la ukame, mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba, hivyo kutojitosheleza kwa chakula. Bila shaka wanapopanda ovyo, wanavuna ovyo. Kuna wakulima ambao hupalilia mmomonyoko Wa udongo kwa kulima kandokando ya mito, kupanda zao lile lile katika sehemu ile ile ya ardhi miaka nenda miaka rudi, na kutopanda mimea ambayo hukinga tabaka la juu la udongo dhidi ya kumomonyolewa na maji au upepo. Matokeo ya haya yanaweza kutabiriwa; udongo wcnye rutuba huoshwa na mashamba kutwaa utasa ambao huzidisha kuzalishwa kwa chakula haba. Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea ambayo hustahimili ukame kama vile mibaazi, mihogo, Intama, ulezi na wimbi. Baadhi ya wafugaji hufuga mifugo Wengi ambao hushindwa kustahimili kiangazi. Si ajabu kupata kwamba katika baadhi ya maeneo, mizoga ya ng’ombe na hata ngamia imezagaa kote, tanuri la kiangazi linapofanya kazi yake.

Sehemu nyingine zimebarikiwa kwa ukwasi wa chakula. Hata hivyo, baadhi ya wakazi Wa sehemu hizi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora. Wapo Wanaodhani kuwa chakula ni chakula, bora tumbo lipate haki. Hawa hula vyakula kama vile viazi, mahindi, na Wengine nyama bila kujua wanahitaji vyakula vyenye virutubisho muhimu, yaani, Wanga, protini, vitamini na madini. Wapo wanaodhani kuwa protini pekee ni nyama. Hawa hula nyama mawio na machweo, matokeo yakiwa kuambulia magonjwa kama vile shinikizo la damu.

Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula, serikali, kupitia wizara husika, imeanzisha miradi ya kuhakildsha kuwa kuna uzalishaji wa chakula kwa kiwango cha kuridhisha. Visirna vya maji na mabwawa yamechimbwa katika sehcmu kame ili kunyunyizia mashamba maji. Baadhi ya wakulima wameanza kupanda mimea ambayo inapevuka na kutoa mazao haraka. Ipo mimea ya kualika ambayo huloa matunda baada ya muda rnfupi, hivyo kusaidia kupunguza makali ya njaa. Wafugaji wengine wameanzisha miradi ya kufuga kuku wa kututumuliwa. Hawa hukua na kukomaa kwa muda mfupi na huweza kutoa nyama na mayai. Wafugaji wa kuku hawa huweza kuwauza kununua aina nyingine ya vyakula.

Wakulima pia wanahimizwa kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula. Chakula kinapohifadhiwa vyema, hata mvua isiponyesha, raia huweza kujitcgcmea. lkiwa maghala ya halmashauri za kuhifadhi chakula nchini hayahifadhi chakula, mara nyingi nchi hulazimika kuagiza chakula kutoka nje kiangazi kinapojiri. Aidha, chakula kisipohifadhiwa vyema huishia kuharibika na kuhasiri wanaokila, ikawa msiba juu ya mwingine.

Ni muhimu kufahamu kuwa jukumu la kupambana na ukosefu wa chakula ni la kila raia. Hali ya kungojea kila mara kulishwa na serikali inatufanya kuwa wategemezi zaidi. Wakulima wadogowadogo ambao huuza vyakula vyao kwa bei ya chini sana mama tu wanapovitoa mashambani Wanapaswa kujiasa dhidi ya mazoea haya na kujua kuwa akiba haiozi. Wanaoishi katika sehemu zenye vinamasi wasaidiwe kuzitunza schemu hizi na kuzitumia kwa njia endelevu. Vijana wahimizwe wawaunge wazee rnkono kushughulikia kilimo katika sehcmu za mashambani badala ya kuhamia mijini kutafuta kazi za ajira ambazo ni haba. Wanaoishi mijini nao wajifunge nira kutumia nafasi Walizo nazo kuendeleza kilimo cha bustani.

(a) Fupisha ujumbe wa aya tano za kwanza kwa maneno 100.

(alama 9, 1 ya mtiririko)

(b) Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, eleza njia sita za kukabiliana na uhaba Wa chakula. (maneno 85)

(alama 6, 1 ya mtiririko)

MATUMIZI YA LUGHA: (Alama 40)

(a) (i) Eleza maana ya silabi. (alama 2)

(ii) Andika neno lenye muundo ufuatao: (alama 1)

irabu + konsonanti + konsonanti + irabu

(b) Ainisha vitenzi katika sentensi: (alama 3)

Ndege yu taabani, hata hivyo anajaribu kujinasua. (alama 3)

(c) Geuza sentensi ifuatayo kwa kufuata maagizo. (alama 2)

Wachezaji hawakucheza mpira kwa sababu ya mvua.

Anza kwa: Mpira

(d) Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali timilifu.

Debi huwapigia watu nguo pasi. (alama 2)

(e) Andika sentensi ifuatayo upya ukizingatia kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)

Ubora wa kazi zao ulifichika baada ya kunzishwa kwa mradi ule.

(f) (i) Eleza maana ya kirai. (alama 2)

(ii) Ainisha virai vilivyopigiwa mstari. (alama 1)

Zana hizi zimeundwa na mafundi wenye ustadi mkubwa.

(g) Kinga ni hali ya kuzuia madhara fulani. Andika maana nyingine mbili za kinga.(alama 2)

(h) Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha matawi. (alama 2)

Lililimwa vizuri sana.

(i) Bainisha maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo: (alama 2)

Wakimbizi walisema kuwa walitamani kurudi kwao mwaka huo.

(j) Eleza sifa mbili za sauti ifuatayo dh. (alama 2)

(k) Andika sentensi ifuatayo katika umoja. (alama 2)

Hao Wenyewe hawakuzingatia mafunzo ya lishe hora.

(l) Tunga sentensi moja kubainisha tofauti ya kimaana kati ya gharama na karama. (alama 2)

(m) Kanusha sentensi ifuatayo

Wanafunzi waliingia darasani, wakatoa vitabu wakaanza kusoma. (alama 2)

(n) Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili tofauti ya nukta pacha. (alama 2)

(o) Tumia nomino ya jamii kuwakilisha maneno yaliyopigiwa mstari.

Nzige wengi sana walivamia na kuharibu mimea. (alama 1)

(p) Onyesha visawe vya maneno yaliyopigiwa mstari.

Washiriki wote walituzwa medali baada ya mchuano huo. (alama 2)

(q)Nomino zifuatazo zimo katika ngeli gani?

(i) Furaha (alama 1)

(ii) Nyasi (alama 1)

(r) Unganisha sentensi hizi ukitumia kiunganishi cha kinyume. (alama 2)

Wananchi walikabiliwa na hatari.

Wananchi waliendelea kuwaokoa majeruhi.

(s) Andika upya sentensi ifuatayo ukianzia kwa yambwa tendwa.

Wafugaji Waliwakatia ng’ombe wote majani ya mti huo. (alama 2)

4 ISIMUJAMII: (Alama 10)

(a) Umepewa jukumu la kuwazungumzia vijana wenzako kuhusu umuhimu wa uwekezaji. Fafanua sifa tano za lugha utakayotumia. (alama 5)

(b) Eleza sifa tano za sajili ya kidini. (alama 5)

Karatasi ya 3

FASIHI

SEHEMU A: RIWAYA

1. Lazima

K. Walibora: Kidagaa Kimemwozea

“Labda ni suala la mzigo wa mwenzio kanda la usufi.” “….Sijui ‘mwenyewe’ aliyetajwa ni nani. Lakini sharti awe mtu ambaye kwake msiba kwa wengine kwake arusi.”

(a) Fafanua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(b) Bainisha‘ tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)

(c) Jadili jinsi ambavyo hali ya, ‘msiba kwa wengine kwake arusi’, inavyojitokeza katika Kidagaa Kimemwozea. (alama 14)

SEHEMU B: TAMTHILIA

T. Arege: Mstahiki Meya

Jibu swali la 2 au la 3.

2. “Waache wagome, Watajiponza Wenyewe.”

(a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama. 4)

(b) Dondoo hili linadokeza mojawapo ya mbinu hasi za ulawala. Iandike. (alama 2)

(c) Fafanua mbinu nyingine saba hasi za utawala zilizotumiwa katika tamthilia hii. (alama 14)

3 “Ngoja ngoja huumiza matumbo.” Thibitisha kauli hii kwa kurejelea tamthilia ya Mstahiki Meya. (alama 20)

SEHEMU C: HADITHI FUPI K. Walibora na S. A. Mohamed: Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine Jibu swali la 4 au la 5.

“Maskini, Babu Yangu!” (K. Walibora)

4 (a) “Salalaa! Mbona wasirudi kwao waishi maisha ya maana kidogo.”

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(ii) Fafanua umuhimu wa mzungumzaji katika hadithi hii. (alama 8)

(b) “Shangazi wakumbuke watoto. Waonee huruma!”

(i) Andika tamathali ya usemi inayojitokeza katika kauli hii kwa kurejelea hadithi:

“Samaki wa Nchi za Joto”. (alama 2)

(11) Bainisha matumizi mengine matatu ya tamathali hii ya usemi katika hadithi hii. (alama 6)

“Maeko” (Mohamed Khelef Ghassany)

5. “Hutaki kuwaeleza, kuwa meridhika, oo ‘ridhika’

Eleza kinyume kinachojitokeza katika maneno yaliyopigiwa mstari kwa kurejelea hadithi hii. (alama 20)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au la 7.

6 Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Amiri A.S. Andanenga: Sauti ya Kiza

1. Ngakua na mato, ya kuonea
Ngalisana kito, cha kuchezea
Kilicho kizito, cha kuelea
Kikamuenea, akivae.

2. Makusudi yangu, ngaliandaa
Ngafinyanga chungu, cha mduwaa
Ngatia vitangu, vinavong’aa
Ili ziwe taa, kwa apikae.

3. Mkungu wa tano, wa mduwara
Ulo bora mno, kisha imara
Ulo na maono, kuwa ni dira
Kwenye barabara, itindiae.

4. Ngaomba baraka, kwake Rabana
Punje za nafaka, kila aipa
Chunguni kuweka, kwa kulingana
Hajaangu suna, yule alae.

5. Ngafanya bidii, kwenda mwituni
Sio kutalii kukata kuni
Ya miti mitii, huko jikoni
Isio na kani, ni iwakae.

6. Kwa yangu rnabega, nikathubutu
Ngabeba mafiga, yalo matatu
Bila hata Woga, kwenye misitu
Simba tembo chatu, sinitishie.

7. Miti yenye pindi, na jema umbo
Ngajenga ulindi, mwema wimbombo
Fundi aso fundi, penye kiwambo
Moyo wenye tambo, agekechae.

8. Singaajiri, ngachimba mimi
Kisima kizuri, cha chcmchemi
Maji ya fahari, ya uzizimi
Jua la ukami, siyaishae.

9. Tamati nafunga, kwa kuishia
Mato ndo malenga, kanikimbia
Nahofu kutunga, mabeti mia
Asije chukia, ayasomae.

(a) Eleza ujumbe Wa shairi hili. (alama 2)

(b) Kwa kurejelea ubeti wa pili, eleza umuhimu wa aina mbili za uhuru wa kishairi alioutumia mshairi.(alama 4)

(c) Andika ubeti wa saba kwa lugha ya nathari. (alama 4)

(d) Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)

(e) Fafanua aina tatu za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 6)

(f) Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)

7. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

T. Arege: Watafuta Riziki

1. Watafuta riziki, watokwa jasho vijijini
Wakulima shakiki, wakuza chai na mibuni
Vyakula wahakiki, visipungue vinyuani.

2. Watafina riziki, wahangaikao mijini
Kutwa kile na hiki; kamawatanga na mipini
Japo hawasikiki, hawakosi kujiarnini.

3. Watafuta riziki,wazalendo Wa nchi hii
Kaniwc hawajidhiki, tamaa za moyo kutii
Bali huafiki, kupingfiha na ulaghai.

4. Watafuta riziki, pate ambalo la halali
Ndoto haizimiki, ya kesho kuwa njema hali
Wiki baada wiki, la haramu jasho hawali.

(a) Fafanua sifa tano za Watu wanaozungumziwa katika shairi hili. (alama 5)

(b) Bainisha umuhimu wa tamathali tatu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 6)

(c) Eleza kwa kutoa mifano, mbinu tatu ambazo mshaifi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 6)

(d) Ainisha shairi hili kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo (alama 3)

(i) idadi ya mishororo katika beti

(ii) mpangilio wa vina

(iii) mpangilio wa maneno

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

8 (a) Soma hadithi ifuatayo kisha ujibu maswali.

Basi Mulungu akamtuma kinyonga duniani kumpasha binadamu ujumbe ufuatao: “Maisha yako hayatakuwa na mwisho, hata ukifa utafufuka.”

Kinyonga akaondoka kama mshenga apelekaye posa. Akatambaa polepole, moyoni amejawa na hofu ya kuiharibu ardhi ya wenyenwe. Hata alipowafikia binadamu machweo ya siku ya saba baada ya kupashwa ujumbe, alimpata mnana keshaubatilisha ujumbe huo; ameisha kumwambia binadamu kuwa akifa atatokomea kama mizizi ya msubili. Huo ukawa ndio mwanzo Wa mauti.

(i) Andika aina ya hadithi hii. (alama 2)

(ii)Fafanua umuhimu wa aina hii ya hadithi katika jamii. (alama 10)

(b) Eleza majukumu manne ya fomyula ya kumalizia katika ngano. (alama 8)